KAMBI Rasmi ya Upinzani Bungeni, imelitaka Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuwafutia posho wabunge wa CCM wanaofika kwenye vikao vya Bunge hilo na kukaa kimya bila kuchangia jambo lolote hata kwa maandishi kwa maelezo kuwa hawafanyi kazi.
Msemaji Mkuu wa Kambi hiyo, ambaye ni Mbunge wa Momba, David Silinde (Chadema), alitoa pendekezo hilo jana bungeni mjini hapa muda mfupi kabla ya kuwasilisha maoni ya Kambi ya Rasmi ya Upinzani Bungeni, kuhusu hotuba ya Mapendekezo ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali katika mwaka wa Fedha 2016/17.
Hotuba hiyo ya Bajeti iliwasilishwa bungeni Juni 8, mwaka huu na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango. Silinde alisema;
“Kabla ya kutoa maoni ya Kambi ya Upinzani, ninaomba niweke sawa taarifa zinazopotoshwa na kiti cha Naibu Spika kuhusu posho na kueleza kuwa sisi ndio kila wakati tumetaka posho ziondolewe na kupelekwa kwenye shughuli za maendeleo, lakini Serikali imekuwa ikisuasua kutekeleza jambo hilo.”
Kwa mujibu wa Silinde, suala kwao sio posho kwa sababu hata wakati wa Bunge la Katiba kila Mbunge wa upinzani aliacha Sh milioni 30.
Akizungumzia wabunge wa CCM wakaa kimya, Silinde alisema wapo na wanapokea posho kama kawaida ilhali hakuna kazi yoyote wanayoifanya na kwamba umefika wakati sasa Bunge liongeze umakini zaidi kwa kuwadhibiti wabunge wa aina hiyo kwa kuwakata posho za vikao.
Alipendekeza kuwa Hansard (kitabu cha taarifa rasmi za Bunge) zitumike kuwabaini kwa sababu wapo na wanajulikana.
Hata hivyo, kabla ya kueleza suala hili, Silinde alivunja utaratibu kwa kumtaja Naibu Spika kwa jina ‘Kiti cha Spika’ badala ya Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lililosababisha alazimishwe kutumia busara kuheshimu kiti hicho na hatimaye kutii.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana,Ajira na Wenye Ulemavu), Jenister Mhagama, ndiye aliyesimama kuomba mtoa hoja (Silinde), aheshimu utaratibu wa Bunge hilo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post a Comment