Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 26 Julai, 2016 amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Frannie Leautier katika Ikulu ya Chamwino Mkoani Dodoma, ambapo ameishukuru benki hiyo kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya Tanzania hususani kutoa mikopo iliyowezesha ujenzi mkubwa wa barabara.
Pamoja na kuishukuru AfDB Rais Magufuli ameiomba benki hiyo kuendelea kushirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa mipango na miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo mpango mkubwa wa uzalishaji wa nishati ya umeme utakaofanikisha ujenzi wa viwanda, ujenzi wa barabara zinazounganisha ndani na nje ya Tanzania na kuunga mkono juhudi za kukabiliana na rushwa.
Kwa upande wake Makamu wa Rais wa AfDB Dkt. Frannie Leautier amempongeza Rais Magufuli kwa juhudi kubwa alizozianza katika kujenga uchumi wa Tanzania, kukabiliana na rushwa na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya serikali na ameahidi kuwa benki hiyo itaendelea kuunga mkono juhudi hizo kwa kutoa mikopo ya masharti nafuu itakayofanikisha mipango na miradi mbalimbali ya Tanzania.
"Tanzania ni nchi ambayo inapata fedha kuliko nchi zote za Afrika katika mpango wa AfDB kupitia Mfuko wa Maendeleo wa Afrika, hizi ni fedha ambazo zinatolewa kwa mkopo nafuu zaidi kuliko mikopo mingine" Amesema Dkt. Frannie Leautier.
Dkt. Frannier Leautier amebainisha kuwa AfDB inatarajia kuwa Tanzania itanufaika kupitia vipaumbele vitano vya benki hiyo ambavyo ni kusaidia uzalishaji wa nishati, utangamano wa bara la Afrika, maendeleo ya viwanda, usalama wa chakula na kuboresha hali ya maisha.
Aidha, Makamu wa Rais huyo wa AfDB amesema kuanzia mwakani benki hiyo imepitisha miradi mikubwa mitatu kwa ajili ya Tanzania ambayo ujenzi wa nyumba ya makazi, utoaji wa mikopo vijijini kwa ajili ya kuendeleza kilimo na maeneo ya uchumi kupitia benki ya CRDB na kukiendeleza Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Nelson Mandela kilichopo Arusha ambapo benki hiyo itatoa Dola za Marekani Milioni 4.
Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Mwakilishi Mkazi wa AfDB Dkt. Tonia Kandiero, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji.
Post a Comment