Bodi ya Wadhamini ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) imesema kuwa haiwezi kuzungumzia lolote kuhusu hatma ya aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Dk Ramadhani Dau kwa vile si mwajiriwa wao.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana kwa simu, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Profesa Samwel Wangwe alisema bodi inashughulika na wafanyakazi wa sasa katika shirika hilo na siyo walioondoka.
“Bodi haiwezi kuchukua hatua dhidi yake (Dk Dau).Vyombo husika ndivyo vitaamua kuhusu hilo,” alisema Profesa Wangwe alipoulizwa kuhusu hatma ya Dk Dau ambaye alikuwa bosi na msimamizi mkuu wa menejimenti iliyosimamishwa kazi.
Pia, katika kipindi ambacho Dk Dau alikuwa mkurugenzi mkuu, aliyekuwa Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi iliyopaswa kutoa idhini ya ujenzi wa kila mradi uliopangwa alikuwa Abubakar Rajabu.
Profesa Wangwe alisema hayo alipoulizwa kuhusu hatma ya Dk Dau baada ya bodi hiyo juzi kuwasimamisha wakurugenzi sita wa shirika hilo na mameneja sita kupisha uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu na matumizi mabaya ya ofisi.
Dk Dau amekuwa mkurugenzi mkuu wa NSSF kwa miaka kadhaa hadi Februari mwaka huu alipoondolewa baada ya kuteuliwa na Rais John Magufuli kuwa balozi, ingawa bado hajapangiwa nchi.
Katika kipindi alichoondolewa NSSF, ripoti ya ukaguzi uliofanywa na kampuni ya Ernst & Young kwa hisani ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ilivuja ikionyesha ubadhirifu wa fedha katika miradi mikubwa ya ujenzi wa majengo ya kisasa yakiwemo ya mji mpya wa Kigamboni jijini Dar es Salaam uitwao Dege Eco Village.
Miradi mingine ambayo ilichunguzwa na CAG akatilia shaka ni ujenzi mradi wa Arumeru, Arusha ambapo NSSF ilikubali kujenga majengo ya kisasa katika viwanja vya mbia mwenzake kampuni ya Azimio Housing Estate Limited ambavyo ekari moja ilithaminishwa kwa Sh1.8 bilioni.
Hata hivyo, mradi huo wenye thamani ya Sh7.2 trilioni ulisimamishwa Januri mwaka huu.
Machi 19, Rais John Magufuli alimteua Profesa Godius Kahyarara kuchukua nafasi ya Dk Dau na Juni 28, Profesa Wangwe aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi. Uteuzi wake ulianza Mei 30.
Bodi ya NSSF, katika kikao cha 106 kilichoketi Julai 15, chini ya Profesa Wangwe ilijadili ripoti mbalimbali na kufikia hatua ya kuwasimamisha vigogo hao ikisema mbali ya ubadhirifu na matumizi mabaya ya ofisi pia wanakabiliwa na tuhuma za kutofuata kanuni, sheria na taratibu za manunuzi katika uwekezaji na usimamizi wa miradi, manunuzi ya ardhi na ajira.
Wakurugenzi waliosimamishwa ni Yacoub Kidula (Mipango, Uwekezaji na Miradi), Ludovick Mrosso (Fedha), Chiku Matessa (Rasimali Watu na Utawala), Sadi Shemliwa (Udhibiti Hadhara na Majanga), Paulin Mtunda (Ukaguzi wa Mahesabu ya Ndani) na Crescentius Magori (Uendeshaji).
Mameneja waliosimamishwa ni Amina Abdallah (Utawala), Abdallah Mseli (Uwekezaji), John Msemo (Miradi), Davis Kalanje (Mhasibu Mkuu), Chedrick Komba (Meneja Kiongozi Temeke) na Mhandisi John Ndazi ambaye ni meneja mradi.
Taarifa zaidi zilizopatikana zilieleza kuwa baadhi ya maofisa wa shirika hilo walifikishwa juzi katika Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) kwa tuhuma ambazo hadi jana hazikuwa zimewekwa wazi.
Mkurugenzi wa Mawasiliano Takukuru Mussa Misalaba alipoulizwa alisema hawezi kusema ndiyo au hapana, lakini hiyo ipo chini ya taasisi hiyo.
“Siwezi kukutajia majina kwamba nani na nani wanachunguzwa na Takukuru, sababu kufanya hivyo ni kuwadhalilisha. Kwa kifupi hiyo ni kazi yetu,” alisema.
Aidha, Profesa Wangwe alisema maofisa hao waliosimamishwa kazi juzi kupisha uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu na matumizi mabaya ya ofisi, watachunguzwa na vyombo kulingana na aina ya makosa yao.
Alipoulizwa kuhusu vyombo vinavyowachunguza maofisa hao alisema hafahamu ni vipi na ni vingapi.
“Vyombo vinavyohusika vitafanya uchunguzi kulingana na aina ya tuhuma zinazowakabili. Siwezi kusema ni vingapi,”alisema Profesa Wangwe.
Kwa mujibu wa ripoti kamili ya CAG, Profesa Mussa Assad iliyowasilishwa bungeni mjini Dodoma Aprili mwaka huu, kuna utata wa ardhi ya mradi mpya wa mji wa Kigamboni unaojengwa na NSSF kwa ubia na kampuni ya Azimio Housing Estate.
Ramani ya mradi huo wenye thamani ya Dola za Marekani 653.44 milioni (Sh1.254 trilioni) inaonyesha utakapokamilika utachangia kubadili sura ya jiji la Dar es Salaam kwani kutakuwa na nyumba za kifahari, majengo ya hoteli, maduka makubwa, eneo la wazi la mapumziko, baa, shule, hospitali, kumbi za mikutano, nyumba za ibada na migahawa.
Profesa Assad katika ripoti hiyo alitilia shaka uhalali wa Azimio kumiliki ekari 20,000 za ardhi ambazo imetoa kama sehemu ya asilimia 20 ya mchango wake katika mradi huo na kwa kuanzia imetoa ekari 300.
“Ukaguzi wa hatimiliki umeonyesha kuwa Azimio inamiliki viwanja viwili, kiwanja chenye hatimiliki Na. 81828 chenye ukubwa wa hekta 1.98 na chenye hatimiliki Na. 105091 chenye ukubwa wa hekta 114.11,” anasema CAG.
“Viwanja vyote vinapatikana katika eneo la Rasi Dege ambavyo kwa pamoja vilihamishiwa kwa Hifadhi Builders kutoka kwa Azimio kwa ajili ya Awamu ya Kwanza ya mradi.
"Kwa kutumia kizio cha ekari 2.47 kwa hekta, hatimiliki hizi zitakuwa na ukubwa wa jumla wa ekari 286.74, pungufu ya ekari 13.26 kutoka kwenye ekari 300 ambazo zilipangwa kwa ajili ya awamu ya kwanza ya mradi,” anafafanua CAG.
CAG anasema katika kipindi chote cha ukaguzi wa mradi huo ulioanzishwa mwaka 2014, hakuwahi kupatiwa hatimiliki za ardhi ambayo Azimio aliahidi kutoa kama uchangiaji wa mtaji.
Vilevile, CAG aliitaka NSSF kuhakikisha inakirejesha katika muda uliopangwa kiasi cha Dola za Marekani milioni 20.1 (Sh43.9 bilioni) ambazo iliilipa Azimio kwa ushauri wa ujenzi wa mradi wa mji wa Arumeru, Arusha.
“Katika ukaguzi imeonekana Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii limepokea upembuzi yakinifu wa mradi pendekezwa kutoka Azimio Housing Estate Ltd kupitia barua yake ya Mei 16, 2013 yenye kumbukumbu Na. Azimio/NSSF/Arumeru/13/5. Bodi ya Wadhamini iliidhinisha kuingiza katika ubia ardhi iliyotolewa na kampuni ya Azimio katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Mwanza na Arusha kwa ajili ya uwekezaji unaofanana na huu,” anasema.
“Ada ya ushauri kwa ajili ya kubuni mradi huo ni Dola za Marekani milioni 218.09 (Sh 468.9 bilioni) na ilipangwa Sh 2.4 bilioni zitumike katika awamu ya upangaji wa mradi. Hata hivyo, kiasi hicho kiliongezwa hadi kufikia Sh 102 bilioni bila ya idhini ya Bodi,” anaeleza.
Kwa kuwa baadaye NSSF na Azimio walikubaliana kufuta mradi wa Arumeru wenye thamani ya Sh 7.2 trilioni huku Sh43.9 bilioni zikiwa zimetolewa, CAG ameitaka NSSF kuhakikisha mbia huyo anazirejesha katika muda wa miaka mitatu kwa kuangalia riba iliyoko katika soko la wakati huo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post a Comment