UMOJA wa Vijana wa Chama cha Wananchi (JUVICUF), umeapa kutotoa ushirikiano wa kikazi kwa viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) walioteuliwa na Rais John Magufuli ambao wanatoa matamko yasiyo na tija kwa wananchi.
Mkuu wa Idara ya Habari na Uenezi wa JUVICUF, Dahlia Majid alisema katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuwa uteuzi wa makada wa CCM katika nafasi za wakuu wa wilaya pamoja na wakurugenzi utavuruga nchi hususani katika kipindi cha uchaguzi.
Akisoma tamko hilo kwa niaba ya Mwenyekiti wa JUVICUF Taifa, Hamidu Bobali, Dahlia alisema viongozi wa awamu ya tano wanakurupuka na kutoa matamko yasiyo na tija yanayobaka mamlaka ya Jeshi la Polisi.
“Haiwezekani viongozi wa awamu ya tano wanakurupuka tu wanatoa matamko yasiyo na tija kila siku tena mengine yanabaka mamlaka hata ya mahakama na wanajifanya wao ndio polisi, wao ndio mahakama na wao ndio magereza, tutawaagiza viongozi wetu katika halmashauri zinazoongozwa na CUF kukataa kauli na matamko ya namna hiyo.
“JUVICUF tunakitaka Chama cha CUF kuwaagiza viongozi wake katika halmashauri tunazoziongoza kwamba waache mara moja kutekeleza maagizo yasiyo na tija kutoka kwa viongozi waliolewa madaraka.
“Tunawasihi vijana waendelee na shughuli zao za kujiletea maendeleo bila kujali matamko yanayotolewa na viongozi waliolewa madaraka na kujifanya miungu watu,” alisema.
Dahlia alitolea mfano wa agizo lililotolewa hivi karibuni na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda la kuwakamata wananchi wasiokuwa na kazi maalumu ambapo alisema hayo ni miongoni mwa maagizo ya ovyo na hayapaswi kutekelezwa.
Kiongozi huyo wa vijana alisema agizo hilo ni kinyume cha sheria huku akitahadharisha kuwa utekelezaji wake utahusisha askari kupiga watu, visa na vijana kubambikiwa kesi zisizokuwa na sababu.
“Ni ajabu sana na hii haipo kote duniani kibali cha kuwakaguwa wananchi majumbani kutolewa na viongozi wa kisiasa, mahakama zina kazi gani? serikali imefanya maisha kuwa magumu na ajira kuwa ngumu kupatikana halafu wao wanaibuka na sera ya kukamata watu wasio na ajira,” alisema Dahlia.
Post a Comment