Mchungaji wa Kanisa la Maombezi (GRC) la Ubungo jijini Dar es Salaam, Anthony Lusekelo maarufu ‘Mzee wa Upako’ amesema kitendo cha viongozi wa CCM kulitaja zaidi jina la Edward Lowassa katika Mkutano Mkuu Maalumu wa chama hicho ni ishara kuwa Waziri Mkuu huyo wa zamani ni tishio.
“Nani! Lowassa…. jina lake kutajwa sana katika vikao vya CCM. Hiyo inaashiria kuwa ni mtu tishio. Ndiyo ni tishio,” alisema Lusekelo jana katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Lusekelo ambaye hivi karibuni, Rais John Magufuli alishiriki ibada katika kanisa lake, alimzungumzia Lowassa baada ya kuulizwa swali juu ya mtazamo wake kuhusu Mkutano Maalumu wa CCM ambao jina la mgombea huyo wa urais kupitia Chadema na Ukawa lilitajwa na makada wengi wa chama hicho tawala.
Alisema hilo lilidhihirika hata katika mchakato wa CCM kupata mgombea wake wa urais, kutokana na Lowassa kuungwa mkono kwa kiasi kikubwa.
Alisema kitendo cha Waziri Mkuu huyo wa zamani kuzua mjadala katika Mkutano Mkuu wa chama hicho tawala sambamba na wimbi la makada wanaohama vyama vyao, si mambo yanayopaswa kuwa mjadala kwa sababu uchaguzi ulishapita.
Huku akisema: “Sizungumzi haya kwa ajili ya kujipendekeza, sihitaji ukuu wa wilaya,” Lusekelo aliwataka viongozi kukataa kuendeleza uhasama wa kisiasa na chuki kwa maelezo kuwa mwaka huu uwe maalumu kuzika tofauti hizo, kufanya kazi kulijenga Taifa na kuhubiri amani na umoja.
Katika mkutano huo, Lusekelo alipongeza kuimarika kwa vyama vya upinzani akaponda mvutano ulioibuka bungeni akisema kukosa uzoefu kwa Naibu Spika, Dk Tulia Ackson kulichangia huku akiunga mkono kauli ya Rais kuzuia shughuli za siasa na kubainisha jinsi Rasimu ya Katiba ya Tume ya Jaji Joseph Warioba, ilivyopendekeza kupunguzwa kwa madaraka ya Rais.
Jumamosi iliyopita, katika Mkutano Mkuu wa CCM mjini Dodoma, uliomalizika kwa Rais Magufuli kuchaguliwa kuwa mwenyekiti, mzimu wa Lowassa ulitawala kutokana na kila aliyepewa nafasi ya kuzungumza ama kumtaja kwa jina au kwa mafumbo.
Mwenyekiti wa CCM aliyemaliza muda wake, Jakaya Kikwete ndiye aliyeanza kuzungumzia hali ya mchakato wa chama hicho kupata mgombea wake wa urais, kuwa ulikuwa mgumu na majaribu makubwa na kwamba wazee walifanya kazi kunusuru hali hiyo.
Katika mchakato huo, CCM ilikata jina la Lowassa katika hatua za awali, jambo lililosababisha kiongozi huyo kuhama na kundi la wanaCCM na kujiunga na Chadema ambayo ilimteua kuwa mgombea wake wa urais.
Hata hivyo, katika mkutano wake wa jana, Lusekelo alisema katika mchakato wa chama hicho tawala kupata mgombea wake wa urais kulikuwa na watu wenye majina makubwa, akiwamo Lowassa na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe.
“Niliwaambia CCM, Membe huwezi kumpuuza, Lowassa naye huwezi kumpuuza maana wanataka madaraka na kwa vyovyote lazima mtapata mtikisiko. Nikawaomba waahirishe suala la kupata Katiba Mpya maana wasingelimaliza na muda ulikuwa mfupi,” alisema na kuongeza: “Kama mwaka huu hautatumika kutibu majeraha yaliyotokea huko nyuma, tutaharibikiwa sana.”
Alisema mchakato wowote wa uchaguzi na kura ya maoni ndani ya vyama huacha mpasuko na watu hutumia dini na ukabila kubaguana, hivyo lazima baada ya uchaguzi mambo hayo yamalizwe.
“Tunapaswa kukumbuka kuwa wote ni Watanzania tusahau uchaguzi. Sasa ni wakati wa kuijenga nchi. Amani inatengenezwa, na Mungu huwapa hekima maana kujenga ni kazi na kubomoa ni rahisi, huu ni mwaka wa uponyaji na kurejesha Taifa pamoja,” alisema Lusekelo.
Alisema kuanza kubagua watu kwa sababu walitoka CCM kwenda Chadema au kutoka Chadema kwenda chama tawala si jambo sahihi huku akitolea mfano mataifa yaliyovurugika kwa kuendekeza siasa za chuki na uhasama.
Yaliyotokea bungeni
Akizungumza yaliyotokea bungeni na kusababisha wabunge wa Ukawa kususia vikao vya Bunge vilivyoongozwa na Dk Tulia, Lusekelo alisema Mtanzania anayejua historia ya nchi yake hawezi kufumbia macho suala hilo.
“Binafsi nawalaumu waliotoka (wabunge wa upinzani) na waliobaki (wabunge wa CCM). Kushindana si kuzuri. Mbatia (James Mbunge wa Vunjo na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi) na wenzake wanapaswa kujua kuwa naibu spika ni mchanga katika siasa waende naye taratibu maana kapewa ubunge tu na kuwa naibu spika,” alisema.
Huku akiponda uamuzi wa Serikali kufuta urushwaji wa matangazo ya moja kwa moja ya Bunge alisema: “Nashangaa wazee kama Salim (Ahmed Salim – Waziri Mkuu mstaafu), Pinda (Mizengo – Waziri Mkuu mstaafu) na Warioba. Sijui walishindwa nini kukaa na wabunge hawa ili kumaliza tofauti zao.”
Alisema si jambo jema kuongoza nchi kwa mabavu na kusisitiza kuwa hata uhuru ulipatikana kwa mazungumzo.
Mchungaji huyo aliusifu utawala wa Rais Magufuli kuwa una kasi kubwa na kwamba licha ya wananchi kulia ukata, watacheka baada ya mwaka mmoja huku akiwananga wanaomponda Kikwete kuwa hawajui mazuri aliyoyafanya.
Awapongeza wapinzani
Akizungumzia nguvu ya vyama vya upinzani, Lusekelo alisema ushindani wa kisiasa umekuwa mkubwa kutokana na kuimarika kwa upinzani: “Chadema ya sasa si ile ya miaka ya 1990. Wanaongoza miji mikubwa na ukiona chama kina wabunge 40 usikipuuze. Hata nguvu ya mfalme ni watu.”
Mikutano ya siasa
Kuhusu kauli ya Rais kusitisha shughuli za siasa hadi mwaka 2020, alisema jambo hilo linaweza kuonekana baya lakini lina unafuu mkubwa, kwamba Kenya wamelifanya na kufanikiwa kumaliza tofauti za kisiasa.
“Hivi watu 10,000 wakiandamana na kusema Magufuli aliiba kura itakuwaje? Tuna askari wa kuwazuia! Nadhani wanasiasa wafanye kazi ya utawala katika vyama vyao. Tutulie kwanza tutibu majeraha. Hakuna jambo baya kama kuwaongoza watu wenye njaa maana hawana la kupoteza,” alisema.
Hata hivyo, Lusekelo alisema Rasimu ya Katiba ilipendekeza Rais kupunguziwa madaraka na huenda madaraka makubwa aliyonayo Rais yakawa sababu ya nchi kuendelea kuwa na amani.
“Kenya kuzuia maandamano ni ngumu sana lakini hapa kwetu hadi Zitto (Kabwe-Kiongozi wa ACT-Wazalendo) alizuiwa kufanya mkutano wa ndani. Kwetu rais ana madaraka makubwa sana,” alisema huku akiwataka polisi kutekeleza wajibu wao vyema, wakikumbuka kuwa nao ni binadamu.
Post a Comment