Wakati Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) unatarajiwa kujadili ajenda kadhaa ikiwamo ya Rais John Magufuli kukabidhiwa uenyekiti wa chama ngazi ya taifa, baadhi ya wajumbe wameanza kupika zengwe kutaka baadhi ya viongozi wa Zanzibar watimuliwe.
Katika mkutano huo uliopangwa kufanyika Julai 23, Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais mstaafu Jakaya Kikwete anatarajiwa kumkabidhi kijiti hicho Rais Magufuli ikiwa ni sehemu ya utamaduni wa chama hicho viongozi kukabidhiana nafasi hiyo kabla ya kumaliza muda.
Marais wastaafu wamekuwa na utamaduni wa kumwachia nafasi ya uenyekiti wa chama Rais aliyeko madarakani kabla ya muda wao wa miaka mitanio kumalizika, kama alivyofanya Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa.
Makabidhiano ya kijiti hicho yatawezekana tu baada ya Rais Magufuli ambaye atakuwa mgombea pekee wa uenyekiti kupigiwa kura nyingi za ndiyo na wajumbe mkutano huo mkuu na hivyo chama kuandika historia nyingine kwa Kikwete kung’atuka katika uongozi wa chama.
Hata hivyo, habari zilizotufikia jana zinasema mbali ya ajenda ya kubadilishana kijiti cha uongozi na kupokea taarifa ya hali ya siasa na mabadiliko ya muundo wa chama, mikakati inasukwa ili baadhi ya viongozi wa sekretarieti ya chama kutoka Zanzibar akiwemo Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Vuai Ali Vuai, wang’olewe kwa kukitelekeza chama.
Habari hizo zinasema Vuai ni miongoni mwa viongozi ambao mwaka 2014 walijikita zaidi katika Bunge Maalum la Katiba (BMK) mjini Dodoma kwa zaidi ya miezi minne (siku 130) na kuacha kufanya shughuli za chama jambo lilosababisha upinzani kutumia nafasi hiyo kujikita zaidi ndani ya visiwa hivyo.
“Sasa ndani ya chama kuna fukuto, inasemekana kuwa kitendo cha wanachama hao kujikita katika Bunge Maalumu la Katiba lililofanyika mwaka 2014 kilisababisha matokeo mabovu ndani ya chama kwa upande wa CCM Zanzibar hivyo inaonyesha wazi Naibu Katibu Mkuu ameshindwa kutimiza wajibu wake hivyo ni lazima wawajibishwe,”kilisema chanzo cha habari hizo.
Bunge hilo lililotarajiwa kukamilisha kazi kwa siku 70, lilianza Februari 18 lakini hadi Aprili 25 lilikuwa halijakamilisha na ndipo liliongezewa siku 60 kuanzia Agosti 5 hadi Oktoba 4. Vuai alikuwa miongoni mwa wajumbe 201 nchini ambao hawakuwa wabunge.
Kiongozi huyo alipoulizwa kama anajua kwamba anashutumiwa na wenzake kwa madai ya kukitelekeza chama hadi kikawa na wakati mgumu wakati wa uchaguzi mkuu, Vuai alisema anajua na kwamba mizengwe hiyo inasukwa na kikundi cha watu wasiozidi 15.
“Suala la kwenda Bunge Maalumu la Katiba mimi kwangu siyo news (habari). Wanaoeneza taarifa hizi nawajua na hawapendi mimi niwe katika nafasi hii kutokana na maovu yao wanayoyafanya,” alieleza Vuai.
“Hili suala la mimi kwenda Bunge Maalumu la Katiba linawauma na kuwakereketa rohoni kikundi fulani... Nilishasema huko nyuma mimi sikujipendekeza kwenda katika bunge hilo, bali nilifuata tarataibu zinazotakiwa.”
Vuai alilisisitiza kuwa yeye kama kiongozi alifanya kazi kwa mujibu wa katiba ya chama na madai ya uchaguzi wa Zanzibar kuwa mgumu alisema suala hilo limeshatolewa ufafanuzi na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha.
Alisema anachojua CCM wana utaratibu wa kubadilisha viongozi baada ya kipindi fulani, hivyo kama viongozi wake wakuu watamwona anafaa kuendelea nafasi hiyo ataendelea kama kawaida na endapo wataona hafai kuendelea yuko radhi nafasi hiyo ichukuliwe na mwingine.
“Kama nitaendelea Inshallah. Lakini nafasi ya unaibu sikuomba, sitokuja kuiomba na siwezi kuing’ang’ania ila najua kuna kikundi hapa Zanzibar kinanifisidi kwa kujipendekeza kwa viongozi na kuongea uongo juu yangu,” alisema.
“Nawaambia hivi, mimi sina tabia ya kujipendekeza nafanya kazi kwa uadilifu kwa mujibu wa Katiba ya chama. Hili ndilo linawaumiza na kueneza chuki dhidi yangu lakini hawanitishi kwa hilo kwa sababu CCM Zanzibar si Vuai,” alieleza.
Vuai alisema kikundi hicho ni cha wanaCCM wa Zanzibar na hakizidi watu 15 na kimekuwa na tabia ya kufanya mambo ya kifisadi kuanzia ndani ya chama hadi kwenye jumuiya za chama na muda ukifika atakitaja hadharani na matendo wanayoyafanya dhidi ya CCM.
“Narudia tena muda ukifika nitawaumbua hadharani. Najua hawanipendi kwa sababu najua ufisadi wao. Mimi sitorudi nyuma na msimamo wangu wa kufanya kazi kwa uadilifu kwa sababu sikupata nafasi hii kwa ufisadi,” alisisitiza.
Habari zaidi zinasema kuwa sekretarieti ya chama hicho kwa sasa inatumia muda mrefu kubuni muundo mpya wa kuirejesha CCM kwenye ushindani ili iweze kukabiliana vilivyo na joto la vyama vingine vya upinzani vinavyoelekea kuwa na ushawishi mkubwa hasa kwa vijana.
Katika muundo huo, viongozi mbalimbali wanatajwa kutolewa katika nyadhifa zao akiwamo Katibu wa Itikadi na Uenezi Nape Nnauye ambaye kwa sasa ameteuliwa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo.
Kwenye mabadiliko hayo, Rais Magufuli anatajwa kujielekeza kwanza kwenye Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ambayo kwa mfumo wa chama hicho ndiyo injini ya mwelekeo na mafanikio ya chama kwa jumla.
Post a Comment