DAVID Kafulila, aliyekuwa Mbunge wa jimbo la Kigoma Kusini (2010-2015) amesema takwimu za kiuchumi zinaonyesha hali ya Tanzania inaendelea kuwa mbaya zaidi chini ya Serikali ya awamu ya tano, anaandika Pendo Omary.
Kafulila ambaye alipoteza ubunge katika mazingira ya kutatanisha katika uchaguzi Mkuu wa mwaka jana ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam katika kongamano lililoandaliwa na Baraza la Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA) ili kuadhimisha siku ya vijana duniani. Kafulila amesema kuwa kwa sasa Tanzania ndiyo nchi inayoongoza kwa deni kubwa Afrika Mashariki ambapo deni la taifa la Tanzania ni 40% ya pato la taifa hali inayoliweka taifa pabaya zaidi kiuchumi.
“Wakati hali ikiwa hivyo kwetu, deni la taifa la Kenya ni 25% ya pato la taifa lao na deni la taifa la Uganda ni 20 ya pato la taifa na bado Rais John Magufuli anaendelea kukopa kwa kasi ya ajabu,” amesema na kufafanua zaidi kuwa;
“Kwa mujibu wa ripoti ya robo mwaka ya Benki ya Dunia katika kipindi cha robo mwaka tu cha utawala wa Rais Magufuli tayari serikali yake imekopa zaidi ya 900 milioni dola za kimarekani ambazo ni zaidi ya Sh. 2 trilioni za kitanzania.”
Kafulila ametahadharisha kuwa kwa kasi ya ukopaji ya Rais Magufuli na serikali yake suala la serikali kujiendesha yenyewe kwa kujitegemea ni ndoto ambayo haiwezi kufikiwa katika miaka ya hivi karibuni.
“Wakati makusanyo yote ya mapato ya serikali hapa nchini kwa mwezi ni 1.2 trilioni, malipo ya mishahara peke yake ni zaidi ya 570 bilioni kila mwezi lakini wakati huo huo serikali ya Tanzania inalipa deni la Shilingi 500 bilioni kila mwezi. Ameeleza.
Kafulila pia amesema licha ya tambo za serikali ya Tanzania kuwa imeongeza ukusanyaji wa mapato lakini fedha katika shughuli za msingi zinazochochea ukuaji wa uchumi kama kilimo zinazidi kufyekwa na serikali.
Ametoa mfano kuwa; Katika sekta ya kilimo Mwaka 2015 serikali ilitoa 78 bilioni kama ruzuku katika mbolea lakini mwaka huu serikali imetoa 10 bilioni tu kama ruzuku katika mbolea.
Lakini pia akisema mwaka jana akiba ya taifa ya chakula ilikuwa zaidi ya tani laki 4 (400,000) lakini mwaka huu akiba ya chakula ni tani elfu sitini na nane pekee (68,000) na wakati huo huo riba katika mikopo ya benki imepanda kutoka 14% ya 2005 hadi 25% kwa mwaka 2015.
Kongamano hilo lenye mada, “kupiga vita umasikini ili kufanikisha uzalishaji na matumizi endelevu” linaendelea muda huu.
Post a Comment