BEKI wa zamani wa klabu ya Manchester United na timu ya Taifa ya England, Phil Neville, amefunguka na kusema kuwa klabu ya Liverpool kutokana na usajili mzuri iliofanya ana imani kuwa msimu huu unaoanza Agosti 13, itafanya vizuri katika Ligi Kuu England.
Neville aliyasema hayo mwanzoni mwa wiki hii wakati akifanya mahojiano na kituo cha Sky Sports na kusisitiza kuwa kikosi cha kocha Jurgen Klopp cha msimu huu kitakuwa ni moto wa kuotea mbali.
“Nina imani kuwa msimu huu klabu ya Liverpool itatoa upinzani mkubwa sana kwa timu zinazoshiriki Ligi Kuu ya England kulinganisha na msimu uliopita ambapo ilimaliza ligi ikiwa katika nafasi ya nane na hii ni kutokana na kwamba imesajili wachezaji wenye viwango bora.
“Ukiangalia Ligi Kuu ya England msimu huu utaona kuna timu kama saba hivi zitakuwa zinagombania katika nafasi za juu, lakini kati ya hizo kuna timu tatu au nne hivi zitakuwa zinapigania kutwaa taji.
“Nadhani Ligi Kuu ya England msimu huu itakuwa ni ligi bora ndani ya uwanja na nje ya uwanja na hii ni kutokana na ubora wa makocha wa timu hizi na wachezaji wenye viwango vizuri vya soka waliowasajili.
“Nikiwa kama mdau mkubwa wa soka na mpenzi wa klabu ya Manchester United, kocha mkuu wa Liverpool, Jurgen Klopp, katika ligi ya msimu huu ni miongoni mwa makocha wanaoonekana kutisha mno kutokana na ubora alionao licha ya kusajili kikosi kizuri.
“Timu zote zinazotegemewa kucheza Ligi Kuu ya England msimu huu zimejiandaa vizuri na kufanya mazoezi ya kutosha huku wakisaidiwa na mafungu ya fedha waliyonayo ambayo yanawawezesha kupata wachezaji bora kutoka kila kona ya dunia.
“Kwa mfano ukiiangalia klabu ya Manchester United kutoka katika nafasi ya tano katika msimamo wa ligi na kuwa bingwa ni vigumu, lakini kutokana na ujio na maandalizi ya kocha Jose Mourinho aliyokwishafanya hadi hivi sasa nina imani kuwa klabu hii itatoa upinzani mkubwa,” anasema Neville.
“Hivyo hivyo kwa kocha Pep Guardiola, kutokana na maandalizi aliyokwishafanya na usajili alioufanya ni dhairi kuwa msimu huu ligi itakuwa na upinzani mkubwa.
“Hivyo nadhani klabu hizi za Manchester United, Manchester City na Liverpool ni timu za kuziangalia mno, lakini nikiwa kama mpenzi mkubwa wa Manchester United, Klopp wa Liverpool ni wa kuogopwa zaidi kwa sababu ni kocha mzuri na katika kikosi chake ameongeza wenye vipaji.
“Liverpool katika kikosi chake cha msimu huu katika kipindi cha joto imeongeza sura mpya na nadhani italeta upinzani mkubwa kama si kutwaa taji,” anasema Neville.
“Miongoni mwa wachezaji waliosajiliwa klabu ya Liverpool ambao wataongeza nguvu ni beki wa kati, Joel Matip aliyetokea Schalke 04 kwa mkataba wa miaka minne, kipa Loris Karius aliyejiunga akitokea Mainz 06 kwa mkataba wa miaka mitano na winga, Sadio Mane, aliyetokea klabu ya Southampton kwa mkataba wa miaka mitano.
“Wengine ni Ragnar Klavan, Alex Wijnaldum waliotokea klabu ya Augsburg ya Ujerumani na Georginio Wijnaldum aliyetokea klabu ya Newcastle United kwa mkataba wa miaka mitano.
“Hivyo utaona kuwa nyota hao wageni wakichanganyika na wachezaji waliokuwepo msimu uliopita Liverpool kuna uwezekano mkubwa wa kufika mbali na si nafasi ya nane kama ilivyomaliza msimu uliopita.
“Pamoja na timu hizo tatu kuwa katika mchuano mkubwa, lakini pia kuna klabu ya Tottenham Hotspur ambayo inanyemelea katika kinyang’anyiro hicho, kwa kweli mimi ni mpenzi mkubwa wa kocha wa klabu hiyo, Mauricio Pochettino.
“Pochettino toka ateuliwe kuinoa timu hiyo msimu wa 2014/2015, imekuwa ikifanya vizuri, kwa sababu ni kocha mzuri na nadhani timu hiyo itaendelea kufanya vizuri,” anasema Neville.
Phil Neville pamoja na kuichezea klabu ya Manchester United kwa mafanikio kwa kipindi cha miaka 10 toka 1995 hadi 2005, pia ameichezea klabu ya Everton na timu ya Taifa ya England kwa kipindi cha miaka 12 toka 1996 hadi 2007 ambapo katika kipindi hicho aliweza kuichezea mechi 59.
Akiwa na klabu ya Manchester United misimu sita toka 1995/1996 hadi 2002/2003 alikuwa ni mmoja wa wachezaji walioiwezesha klabu hiyo kutwaa taji la ubingwa wa England, FA misimu mitatu 1995/1996, 1998/1999, 2003/2004 na taji la Ngao ya Jamii 1996, 1997, 2003 na taji la UEFA 1998/1999.
Neville alizaliwa Januari 21, 1977 katika mji wa Bury, Manchester, England.
Post a Comment