Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli,jana tarehe 08 Februari, 2017 alifanya ziara ya kushtukiza katika mradi wa ujenzi wa jengo jipya la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam (Terminal 3) na kuagiza shughuli za ujenzi wa uwanja huo ziendelee kuanzia leo.
Awali Mkandarasi anayejenga uwanja huo ambaye ni kampuni ya BAM International alitangaza kusitisha ujenzi kuanzia jana kutokana na kutolipwa madai yake na Mhe. Rais Magufuli ameahidi kulipa fedha hizo haraka.
Hata hivyo, Mhe. Rais Magufuli ameelezea kusikitishwa kwake na namna mradi huo unavyotekelezwa ikiwemo Serikali kukubali gharama kubwa za mradi ambazo ni Shilingi Bilioni 560 kiwango ambacho ni kikubwa ikilinganishwa na jengo linalojengwa.
“Hivi kulikuwa na sababu gani za nyinyi wataalamu wa Serikali kukubali gharama kubwa namna hii, hivi hili jengo linafanana na Bilioni 560?
“Halafu mlikuwa na haraka gani kuidhinisha kuanza awamu ya pili ya ujenzi kabla ya kumaliza awamu ya kwanza?” amehoji Mhe. Rais Magufuli alipokuwa akiwauliza Wahandisi wa Wizara ya Ujenzi wanaosimamia ujenzi huo.
Kufuatia hali hiyo, Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Prof. Makame Mbarawa Mnyaa aliyeongozana nae kuunda timu ya wataalamu watakaofanya tathimini ya utekelezaji wa mradi huo ikiwa ni pamoja na kuzungumza na Mkandarasi anayejenga uwanja huo na Mhandisi Mshauri ambao wamekubali kupunguza gharama za ujenzi wa mradi huo.
“Serikali italipa fedha ambazo Wakandarasi wanadai lakini, nataka Waziri uunde timu ya kufanya tathmini upya, ni lazima hii gharama ipungue, hatuwezi kumaliza fedha zote hizi wakati jengo halifanani na thamani hiyo” alisisitiza Dkt. Magufuli.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ambaye ameonesha kutofurahishwa na dosari zilizoanza kujitokeza katika baadhi ya maeneo ya jengo hilo, amemuagiza Mhe. Waziri Mbarawa kuunda upya timu ya Wahandisi watakaosimamia mradi huo na ambao watafanya kazi kwa uzalendo na kusimamia ubora.
Kabla ya kuondoka uwanjani hapo Mhe. Rais Magufuli alikutana na wafanyakazi walioajiriwa katika shughuli za ujenzi wa uwanja huo na kuwahakikishia kuwa Serikali imechukua za kuhakikisha mradi huo unaendelea na kwamba kuanzia leo wataendelea na kazi kama kawaida.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amemsimamisha kazi Kaimu Katibu wa Tume ya Mipango (Wizara ya Fedha)Bi. Frolence Mwanrialiyeidhinisha kuanza kwa awamu ya pili ya ujenzi wa jengo hilo jipya la Uwanja wa Ndege kabla ya kumalizika kwa awamu ya kwanza ili kupisha uchunguzi.
Mhe. Dkt. Magufuli ameviagiza vyombo vinavyohusika kufanya uchunguzi katika mradi huo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post a Comment