WASANII waliokuwa wa Kundi la Mama ongea na Mwanao ambalo lilikuwa maalumu kwa ajili ya kampeni ya Mgombea Mwenza wa Urais wa CCM 2015, Samia Suluhu Hassan, wamemgeuka Miss Tanzania 2006, Wema Sepetu na kudai kuwa msanii huyo kuwa ni muongo, kwa vile hakuna msanii anayedai kwa kazi hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Mwenyekiti wa kundi hilo, Yobnesh Yusuf maarufu ‘Batuli’ amesema inashangaza Wema kusema anadai fedha wakati yeye ndio aliyekuwa mshika mkoba.
“Kwenye msafara wa mamba na kenge wamo, yeye ndio aliyekuwa anashika fuko la pesa, yeye ndio aliyekuwa anatulipa sisi hela, mikataba ipo, hakuna anayedai na haiwezekani eti atulipe sisi yeye asijilipe ni muongo,” ameeleza Batuli na kuongeza:
“Yeye asitegemee sisi tutamuunga mkono kwenye ‘movement’ zake. Kaamua kuondoka aondoke kwa amani, asiseme uongo na kufanya ugomvi wake kuwa ni wa wasanii wote. Sisi ni makada wa CCM na bado tupo sana, hatufikiri kutoka leo wala kesho.
“Ni aibu kwa msanii mkubwa kama Wema kusimama mbele ya hadhara na kuongopa hajalipwa, hapo anaichafua CCM, anamchafua na Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu ambaye tulikuwa chini yake.”
Batuli amesema hayo kwa niaba ya wasanii wenzake ambao aliongozana nao akiwemo Ndumbagwe Misayo 'Thea', Sabrina Rupia ‘Cathy’, Mayasa Mrisho ‘Maya’, Asha Mzuzuri ‘Asha Boko,’ Halima Yahya 'Davina' na Bi Staa ‘Mama Kibakuli.’
Kundi la Mama Ongea na Mwanao lilizinduliwa Agosti 20, 2015 na Rais mstaafu Jakaya Kikwete, likiwa na lengo la kumsapoti Samia, aliyekuwa Mgombea Mwenza wa Dk John Magufuli, ambaye kwa ushindi wa CCM katika uchaguzi huo, amekuwa mwanamke wa kwanza kuwa Makamu wa Rais tangu Tanzania ilipopata uhuru mwaka 1961.
Wasanii hao wa filamu walizunguka mikoa mbalimbali kipindi cha kampuni, lakini wiki iliyopita Wema akitangaza kuhamia Chadema alidai kuwa kundi lote la Mama Ongea na Mwanao, hawakulipwa fedha zao kwa kazi waliyoifanya.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post a Comment