BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imesema jumla ya wanafunzi 2,348 wameshinda katika kesi zao za rufaa ya mikopo ya elimu ya juu, kati ya wanafunzi 20,020 waliowasilisha rufaa zao kwa bodi hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo, Abdul-Razaq Badru, wanafunzi hao walikata rufaa kutokana na ukweli kuwa taratibu za upangaji na utoaji mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, zinatoa fursa kwa waombaji waliokosa au kupata kiwango wanachoona hakikidhi kukata rufaa.
Alisema kwa mujibu wa taratibu zilizopo, waombaji hupewa siku 90 kuanzia mwanzo wa mwaka wa masomo kuwasilisha rufaa zao na rufaa hizo huwasilishwa kwa njia ya mtandao na vielelezo/viambatisho huwasilishwa kupitia madawati maalumu ya mikopo vyuoni.
“Katika mwaka wa masomo 2016/17, utaratibu wa kupokea rufaa ulianza rasmi tarehe Novemba mosi, mwaka jana na kuhitimishwa Januari 31, mwaka huu,” alisema 2017.
Alisema katika kipindi hicho jumla ya rufaa 20,020 ziliwasilishwa kwa njia ya mtandao na kati ya rufaa hizo jumla ya fomu za rufaa 17,020 zilipokelewa kutoka vyuoni zikiwa na viambatisho muhimu.
Alisema mapitio ya rufaa zilizowasilishwa yalifanywa kwa fomu zote zilizopokelewa na matokeo ya rufaa hizo zilizoshinda kwa makundi ni kama ifuatavyo: Walemavu 61; Yatima 57; Wenye mzazi mmoja 570; Familia zenye kipato duni 1,169 na waliosomeshwa na wahisani 491.
Kutokana na matokeo hayo, Mkurugenzi huyo alibainisha kuwa tayari majina ya wanafunzi walioshinda rufaa zao yametumwa kwenye vyuo vya wanafunzi hao husika na inaendelea kukamilisha malipo ya mikopo yao.
“Aidha, Bodi inapenda kuwataarifu waombaji na umma kwa ujumla kuwa utaratibu wa kupokea rufaa umefungwa rasmi hadi hapo utakapotangazwa tena katika mwaka ujao wa masomo,” alifafanua.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post a Comment