SERIKALI imezindua mashine mpya tatu za ukaguzi wa mizigo bandarini zenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 20.2 zinazotarajiwa kuongeza mapato sanjari na kudhibiti dawa za kulevya, usafirishaji wa wanyamapori na pembe za ndovu.
Akizindua mashine hizo jana katika Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Dar es Salaam, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa alisema mashine mbili zitakuwa kwa ajili ya Bandari ya Dar es Salaam na moja itakuwa katika Bandari ya Tanga.
“Mashine hizi zimetolewa kwa msaada wa Serikali ya China... Tunawashukuru sana hawa wenzetu kwa kuwa wametusaidia kwa mengi na ushirikiano wao umekuwa ukisaidia pia katika kukuza uchumi wa nchi yetu,” alisema Profesa Mbarawa.
Alisema pia wamesaidia mafunzo kwa wataalamu wa TPA, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Kamisheni ya Mionzi iliyopo Arusha ambao ndiyo watakuwa wasimamizi wa mashine hizo.
“Nasisitiza tuwe waadilifu katika kazi kwa sababu bila uadilifu mashine hizo zinaweza zisitusaidie... mtu unaweza ukawa na mashine hizi lakini ukaachia makontena yakapita bila kukaguliwa, hivyo uadilifu na uzalendo ndivyo vitakavyotusaidia,” alibainisha waziri huyo.
Alisema katika uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano, uadilifu ndiyo jambo kubwa hivyo watahakikisha wanazisimamia mashine hizo ili zifanye kazi kwa tija na zikitumika ipasavyo, nchi itaweza kupiga hatua kubwa katika ukusanyaji wa mapato, itawezesha kupambana na dawa za kulevya na usafirishaji wa wanyamapori.
Aidha, alisema serikali ipo katika utaratibu wa kuagiza mashine nyingine sita ili kuhakikisha kila bandari inakuwa na mashine hizo na kuongeza mapato na kuchangia uchumi wa nchi.
Alitoa mwito kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuhakikisha mashine hizo zinatunzwa vizuri na kufanyiwa matengenezo yanapohitajika kabla hazijaharibika.
Mapema Balozi wa China nchini, Dk Lu Youqing alisema Bandari ya Dar es Salaam imetoa mchango mkubwa kwa uchumi wa maendeleo katika nchi nyingi za Afrika na inategemewa kufanya mapinduzi makubwa ya kiuchumi kutokana na maboresho yanayofanyika.
Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Deusdedit Kakoko aliahidi watazisimamia mashine hizo ili zifanye kazi kwa malengo yaliyokusudiwa na kuongeza ufanisi wa Bandari.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post a Comment